Sunday, 24 July 2016

Jifunze Kilimo Bora cha Vitunguu

Vitunguu ni zao la pili ambalo hutumika karibu kila siku katika mlo wa familia za kitanzania. Afrika Mashariki, na Dunia Nzima. 
Vitunguu vina chukua nafasi kubwa katika matumizi ya mboga hasa kwa wakazi wa mijini. Vitunguu hutumika katika kutengeneza kachumbari, kiungo cha mboga, nyama na samaki. Majani ya kitunguu hutumika kama mboga. Vitunguu pia hutumika kutengeneza supu n.k

Aina Za kilimo Cha Vitunguu
Kilimo cha vitunguu kinaweza kufanyika kwa aina mbili
  •   Green House
  •  Shambani 
Kilimo cha kitunguu Green House
Kilimo cha vitunguu katika shamba la kawaida.

Mahitaji muhimu katika kuzalisha zao la vitunguu
Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye maeneo yasiyo na mvua nyingi sana, yenye baridi kiasi wakati wa kiangazi na yasiyo na joto kali pamoja na ufukuto wa ukungu wakati wa kukomaa vitunguu.

Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha. Udongo unao ruhusu mizizi kupenya kirahisi, unao hifadhi unyevu kama vile udongo wa mfinyanzi tifutifu.
Kutayarisha shamba
Shamba litayarishwe sehemu usiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa
vitunguu kwa muda wa miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya
umwagiliaji. Matuta 1m x 3m au majaruba ya 2mx 3m.yanafaa kwa kupanda miche. Matatu au
majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.
Upandaji wa mbegu za vitunguu
Mbegu zinaweza kupandwa kwa mstari au kwa kutawanya katika tuta la kitalu. Katika upandaji wa mstari, mbegu hupandwa katika nafasi ya cm 10 hadi 15 kati ya mstari na mstari. Baada ya kupanda, mbegu hufunikwa kwa udongo na baadaye kwa kuweka matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota, matandazo yaondolewe na badala yake kichanja cha nyasi kijengwe ili kuiwekea kivuli mimea michanga. Mbegu huota baada ya siku 7 hadi 10.
Matunzo ya bustani ya vitunguu
  • Umwagiliaji

 Zao la vitunguu linahitaji maji ya kutosha katika kipindi chote cha ukuaji wa mmea na hasa wakati wa kutunga tunguu. Katika kipindi kisicho na mvua (mwezi mei hadi Agosti) Umwagiliaji ufanyike mara moja kwa wiki kwa udongo wa mfinyanzi tifutifu na vitunguu vilivyopandwa katika vijaruba. Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu unashauriwa kupunguza kiasi cha maji ya kumwagilia taratibu kadri zao linavyo kua. 
Pia ni vizuri uache kumwagilia maji mapema wiki nne hadi sita kabla ya kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa na kuvuna kwa vitunguu ni siku 90 hadi 150 kutegemea na aina ya mbegu. Kuthibiti magugu na kupandishia udongo Kitunguu ni zao lisilo weza kushindana na magugu. Magugu husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza magonjwa na husababisha kudumaa kwa vitunguu. Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kutolewa kwa njia ya kutifulia kwa jembe dogo, kung'olea kwa mkono na pia kwa kutumia madawa ya kuua magugu.
Kama unaondoa magugu kwa kutifulia, epuka kutifua kwa kina kirefu ili kutoharibu mizizi na vitunguu vyenyewe, kwani mizizi ya vitunguu ipo juu juu sana. Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kuwa mashina ya vitunguu vyako ndani ya udongo kama sentimita 5. Pia kuna aina ya vitunguu ambavyo hutoa au hupandisha tunguu lake juu ya udongo wakati vinapokua. Hivyo kupandishia udongo ili kufunika tunguu ni muhimu sana.
Hali ya hewa na maji
Hali ya hewa na maji ni vipengele muhimu sana vya kuzingatia katika uzalishaji wa vitunguu.
Vitunguu vinastawi vizuri katika hali ya ukavu kwa kutumia umwagiliaji. Maji mengi hasa
wakati wa masika inasababisha magonjwa mengi hasa ukungu, vitunguu haviwezi kukomaa
vizuri, hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mazao. Jua na hewa kavu ni muhimu sana wakati
wa kukomaa na kuvuna vitunguu.
Aina za vitunguu
Aina bora za vitunguu ni pamoja na Mang’ola red, Red creole na Bombay Red. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mazao mengi kuanzia 40-60kgs kwa hekta. ikiwa kilimo bora kitazingatiwa. Mkulima anaweza kuchagua mbegu kwa kuzingatia:-
  • Mahitaji ya soko (vitunguu vyekundu hupendwa zaidi)
  • Msimu wa kupanda
  • Uwezo wa kuzaa mazao mengi
  • Uwezo wa vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu.
Mbegu bora

Ubora wa mbegu ni muhimu sana, kwani ndiyo chanzo cha mazao bora. Mbegu bora inatoa miche yenye afya na kuzaa mazao mengi na bora. Mbegu za vitunguu inapoteza uoto wake upesi baada ya kuvunwa (mwaka1). Mbegu nzuri zina sifa zifuatazo:-


  • Uotaji zaidi ya 80%
  • Mbegu safi zisiyo na mchanganyhiko
  • Zimefungwa vizuri kwenye vyombo visivyopitisha hewa na unyevu.
Hivyo mkulima anaponunua mbegu za vitunguu azingatie yafuatayo:
  • Chanzo cha mbegu
  • Tarehe ya uzalishaji
  • Tarehe ya kuisha muda wa
  •  Kifungashio cha mbegu.
Inashauriwa mkulima asipande mbegu zenye umri zaidi ya mwaka mmoja
Mbegu bora za vitunguu zinauzwa na makampuni binafsi kama: 
  •  ALPHA Seed Co, Popvriend,
  • · Rotian Seed, 
  • ·  Kibo Seed, 
  • ·   East African Seed Company nk. 

 Wasambazaji wa mbegu ni pamoja na maduka ya TFA, na maduka ya pembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali.
Magonjwa na wadudu waharibifu wa vitunguu
Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali na kusababisha upungufu na
ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za
mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua za kuzuia kabla uharibifu
mkubwa haujatokea.
Wadudu waharibifu
Kuna aina tatu (3) za wadudu wanao haribu zao hili:
Viroboto wa vitunguu
Hawa ni wadudu waharibifu namba moja wa zao la vitunguu hapa nchini Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wa mavuno. Wadudu hawa huonekana hasa wakati wa kipindi cha joto.
Dalili za kugundua
Majani yaliyo shambuliwa na wadudu hawa huwa na mabaka meupe yenye kung'aa. Katika hali iliyo kithiri majani yote hugeuka kuwa na tabaka nyeupe au kijivu cheupe na baadaye majani hunyauka kabisa.
Kuzuia
Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa kama vile thiodan-35, Parathion nk.


  •       Ili kupunguza uvamizi mkubwa, panga upandaji wa vitunguu mapema ili kipindi cha joto kiingiapo zao lako    liwe limekomaa.
  •       Epuka kupanda zao la vitunguu sehemu iliyo kuwa na mazao aina ya vitunguu kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k. Wadudu wengine waharibifu wa vitunguu ni funza anayekata miche na minyoo ya mizizi.
  •        Hawa hupigwa vita kwa kuzingatia mzunguko wa mazao bustanini.

Chawa wekundu. (Thrips)
Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekundu. (Thrips) ambao wanashambulia majani,
Uharibifu uletwao na wadudu chawa, unatofautiana msimu mmoja na mwingine kutegemeana na
hali ya hewa. Mvua kidogo pamoja na joto kali unasababisha mlipuko wa wadudu.
Wanashambulia majani kwa kukwarua kwarua na kunyonya maji hivyo kusababisha majani kuwa
na rangi ya fedha/siliver na baadaye majani yanakauka. Upungufu mkubwa wa mazao unatokea.

Njia ya kudhibiti hawa wadudu ni:-

  •       Kuweka shamba katika hali ya usafi
  •       Kuondoa magugu shambani na yanayozunguka shamba la vitunguu
  •       Kupulizia dawa ya wadudu kama karate, selecron, dursban, actellic.
Sota (cutworms)  
Sota au viwavi wa nondo wanasababisha uharibifu mkubwa. Viwavi wanakata mashina ya miche
michanga sehemu ya chini ya shina juu ya ardhi. Sota wanapendelea kula wakati wa usiku na
mchana kujificha kwenye ardhi karibu sana na sehemu waliokata shina. Uharibifu huu
unapunguza sana idadi ya mimea shambani na kuleta upungufu wa mazao.
Wadudu hawa wanadhibitiwa kwa kupulizia dawa kama; Karate Dursban na Actellic na kuweka
shamba katika hali ya usafi.
Utitiri wekundu (Red spider mites)
Hawa ni wadudu wadogo sana, ambao wanajificha upande wa chini wa majani. Wanafyonza
maji kwenye majani na kusababisha majani kuwa na rangi nyeupe. Wadudu hawa
wanatengeneza utando mweupe kuzunguka majani na mashina. Mmea unashindwa kutengeneza
chakula na baadaye inakufa.
Njia ya kudhibiti:

  •       Kupulizia dawa za wadudu Karate na Selecron.
  •       Kuteketeza masalia ya mazao
  •       Kutumia mzunguko wa mazao
Vipekecha majani (leaf miner)
Hawa ni aina ya inzi wadogo, ambao viwavi wake wanashambulia majani, kwa kupekecha na
kutengeneza mitandao wa mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na
kusababisha majani kukauka. Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.
Njia ya dhibiti:
·         Kupulizia dawa ya wadudu kama karate Selecron na Dursban
·         Kuteketeza masalia ya mazao
·         Kutumia mzunguko wa mazao
Magugu
Miche ya vitunguu, huota taratibu sana, hivyo miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na
magugu. Palizi mbili mpaka tatu zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya
dawa za magugu ni madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen
(Goal 2E). Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua magugu aina mbalimbali. Dawa
Inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya kupandikizwa miche shambani. Palizi baada ya
kutumia dawa ya magugu ni muhimu ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu.
Wakati wa palizi, vitunguu na mizizi iliyowazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze
mizizi au kubabua vitunguu


Magonjwa ya vitunguu
     a)     Ukungu mweupe
Ugonjwa huu hujionyesha kipindi cha baridi iliyo ambatana na unyevunyevu mwingi hewani.
Dalili za kugundua Ugonjwa huu

  •       Utaona unga wa rangi ya zambarau katika majani.
  •      Majani hugeuka rangi na kuwa njano na baadaye kunyauka.
  •       Ugonjwa huu hupenya hadi chini kwenye tunguu na kusababisha kuoza kwake.
Kuzuia

  •     Inashauriwa kubadili aina ya zao katika shamba lako kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii ya vitunguu. Kilimo cha mzunguko wa aina mbalimbali za mazao upangwe kiasi kwamba vitunguu visipandwe eneo moja mpaka baada ya miaka 3 kama ugonjwa ulikuwa mwingi.

  •       Tumia dawa za kuzuia ukungu. Hii ifanyike kabla ya kuona dalili za ugonjwa kwenye vitunguu. Piga dawa kama vile maneb, Dithane M45, zineb ya unga, n.k. Wakati unapoona hali ya hewa inayo wezesha kuenea kwa ugonjwa huu (yaani baridi iliyo ambatana na unyevunyevu mara kwa mara). Katika kipindi hiki piga dawa kila baada ya siku sita ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa. Ugonjwa ukisha ingia kwenye mimea hauzuiliki kwani hakuna dawa ya kuponyesha.
b) Ukungu wa kahawia
Ugonjwa huu unaweza kuleta madhara makubwa wakati vitunguu vikiwa bustanini na hata wakati vikiwa katika ghala.
Dalili zake
Vikovu vya mbonyeo hujitokeza kwenye majani na baadaye hutoa doa la rangi ya zambarau. Vikovu hivi hukua na kutengeneza vidonda ambavyo hukua na kufanya mzunguko katika jani zima au shina la kitunguu. Baada ya wiki kama tatu hivi tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani yote huanguka na kukauka. Ugonjwa huu hushambulia vitunguu hata baada ya kuvuna kwa kupitia shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu,
kidonda au mkwaruzo.

Namna ya kuzuia
  •       Katika bustani, mara uonapo kitunguu chenye dalili za ugonjwa huu, ondoa mimea na kuiteketeza kwa moto ili kuzuia au kupunguza kuenea kwa ugonjwa.
  •       Kwa kinga ya bustani, piga dawa za Dithane M 45 na dawa zingine za kuzuia magonjwa ya ukungu. Dawa hizi zitasaidia kupunguza kutawanyika kwa ugonjwa.
  •       Tumia kilimo cha kuzungusha au kubadilisha mazao katika eneo la bustani yako. Usipande mfululizo jamii yoyote ya vitunguu katika shamba ulilovuna vitunguu.
  •       Wakati wa kuvuna, epuka kukata au kusababisha vidonda katika vitunguu, yaani vuna kwa kung’olea na siyo kwa kuchimba na jembe.
  •       Baada ya kuvuna anika vitunguu juani kwa siku moja au mbili kabla ya kuviweka katika magunia au ghala.
c) Ugonjwa wa kuoza mizizi
Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na unasababishwa na vimelea vya jamii ya ukungu.
Dalili
Dalili za ugonjwa huu ni mizizi kugeuka rangi na kuwa njano na baadaye kuwa zambarau. Baada ya muda ugonjwa huenea na mizizi hufa kwa kunyauka. Majani nayo hugeuka kuwa na rangi ya njano na kisha shina au mche mzima hunyauka.
Kuzuia

  •       Tumia kilimo cha kuzungusha mazao badala ya kupanda vitunguu katika eneo moja toka msimu moja hadi mwingine.
  •       Panda aina za vitunguu zinazo vumilia ugonjwa huu kwa mfano: Excel, L 36, Granex, White Granex na red creole.
 Kuweka mbolea

Vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha.

• Tumia mbolea za asili ili kurutubisha udongo kwa lengo la kupata mazao mengi na bora. • Iwapo ni lazima kutumia mbolea za viwandani muone mtaalam wa kilimo ili akuelekeze namna ya      kutumia. Mbolea ikizidi huharibu ubora wa vitunguu.



Kumwagilia maji

• Kagua shamba kuona kama udongo una unyevu wa kutosha. Iwapo unyevu ni mdogo mwagilia maji   kufuata mahitaji ya mmea. Vitunguu vinapoanza kukomaa punguza kumwagilia ili kuepuka kuoza




Kudhibiti magonjwa na wadudu


Vitunguu hushambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali ambao huweza kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo hilo kagua shamba mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua tahadhari ya kunyunyuzia dawa mapema kabla madhara hayajaleta upotevu mkubwa.



Kukagua shamba

• Kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa. Vitunguu huwa tayari kuvunwa miezi          mitatu hadi mitano tangu kusia mbegu kutegemea aina ya mbegu na hali ya hewa.Dalili za vitunguu    vilivyokomaa:

• Majani hunyauka na kuanza kukauka
• Asilimia kumi hadi 20 ya mimea huanguka majani na shingo hulegea.
• Majani hubadilika rangi kuwa ya manjano na baadaye kaki



Kuvuna
Vitunguu vinapaswa kuvunwa mapema mara tu vinapokomaa ili kupata mazao mengi na bora.Uvunaji hufanyika kwa mikono ambapo jembe uma hutumika kuchimbua au kulainisha udongo.Udongo ukishalainishwa vitunguu hung’olewa kwa mkono. Inashauriwa uvunaji uanze asubuhi ili vitunguu viweze kunyauka na kukomaza ngozi sehemu za michubuko. 

Vitunguu visiwekwe juani na inapobidi kukomaza ngozi shambani, majani ya vitunguu yatumike kufunika vitunguu ndani ya matuta yake wakati wa mchana ambapo kuna jua. Kusanya vitunguu kwenye vikapu kisha vipeleke sehemu ya kukaushia. 

Vitunguu vya kukaushia kwenye kichanja ni bora zaidi, mizizi na majani hupunguzwa na kuachwa urefu wa robo inchi . Vitunguu vya kukausha kwa kunining’iniza havikatwi majani bali hufungwa kwenye mafungu na kupelekwa sehemu ya kukaushia.

Asanteni sana kwa haya machache yanayoweza kutusbabishia mavuno makubwa katika kilimo chetu cha kitunguu.

somo lijalo tutaweza kuona jinsi ya kutambua magonjwa yanayopata vitunguu na dalili zake.

0 comments: